11/08/2026
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewapa wamiliki na waendeshaji wa Kampuni za Mabasi makubwa ya Mikoani wiki moja kuhakikisha wanaanza kurejesha huduma zao katika Stendi ya Magufuli, isipokuwa kampuni 6 ambazo tayari zina vibali vya kushushia kati kati ya mji, ikiwa ni hatua ya Serikali kupunguza msongamano wa magari katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Chalamila amesema mabasi hayo yanapaswa kuanzia na kumalizia safari katika Kituo cha Magufuli, badala ya kuingia katikati ya jiji kwa ajili ya kupakia na kushusha abiria.
Amesema wamiliki na waendeshaji wa mabasi hayo wanapaswa kutumia muda kuanzia sasa hadi Agosti 17, 2026 kuhakikisha magari yao yanaanza kutumia Stendi ya Magufuli, huku utekelezaji wa utaratibu huo ukianza rasmi baada ya tarehe hiyo.
Kwa mujibu wa Chalamila, abiria wanaofikishwa Stendi ya Magufuli wataendelea na safari zao kuelekea maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam kwa kutumia usafiri wa ndani, ikiwemo mabasi ya mwendokasi, daladala, bajaji na pikipiki au 'shuttle' ambazo zitatolewa na kampuni za mabasi husika
Chalamila amesema hatua hiyo pia inalenga kulinda fursa za ajira na biashara kwa waendeshaji wa usafiri wa ndani, akisema mabasi makubwa yanapoingia katikati ya jiji yanaingilia shughuli zinazoweza kufanywa na wadau wengine katika mnyororo wa usafirishaji.